Hakuna jibu la moja kwa moja ambalo linaelezea mtu anawezaje kuwa mwongozaji wa filamu.“ How to be a Proffessional Film Director”
Swali la msingi kujiuliza ni kwamba mwongozaji “ Director” hasa ni nani katika tasnia ya filamu/sinema? jibu lake laweza kuwa ni fupi, ni mtu anayetengeneza taswira ya namna ya kuwasilisha muswada (script) kuwa maisha halisi, anachagua na anawaongoza wahusika kuweza kuwasilisha ujumbe kama ulivyokusudiwa,
Watu wengi wamekuwa wakitamani au kuwa na Ndoto za kuwa waongozaji wenye mafanikio na maarufu kama James Cameroon, Michael Moore, Mery Gibson, Tsai Ming – Ling, Ang Lee, George Lucas, Tim Burton na wengine wengi. Lakini mafanikio hayo mtu anaweza kuyapata kwa namna gani?.
Mtu anawezaje kuwa mwongozaji wa filamu? Hakuna jibu lolote la kujitosheleza ambalo lipo na linaelezea ni kwa namna gani mtu anaweza kuwa mwongozaji wa filamu. Ingawa unaweza Kusema kuwa mtu anaweza kuwa mwongozaji wa filamu kwa kuchukua video kamera na kuanza kuongoza.
Swali la msingi hapa ni kwa jinsi gani mtu anaweza kuwa mwongozaji mweledi? “A Professional film director”.
1. Mapenzi binafsi ya kuingia kwenye tasnia ya filamu.
Ni dhahiri kwamba wale wote wanaotaka kuwa waongozaji wazuri wa filamu ni lazima wawe na malengo, moyo wa kujituma, ubunifu, uvumilivu, waweze kupokea changamoto kutoka kwa wadau mbalimbali wa filamu na kuzifanyia kazi ili waweze kufanikiwa na kufanya vizuri katika tasnia hii pana na yenye ushindani na changamoto nyingi.
Kabla hata ya kwenda kwenye shule ama vyuo vinavyofundisha mambo ya filamu na uongozaji wa filamu ni muhimu mtu akaanza kwa kujifunza yeye mwenyewe kwa kuangalia filamu/ sinema nyumbani ama kwenye majumba ya sinema, na sinema zinazoangaliwa lazima ziwe na ubora, isiwe mradi simema/filamu.
kusoma vitabu vinavyoelezea historia ya filamu, kufuatilia mitandao mbalimbali inayoandika habari kuhusu mambo ya filamu na kuhudhuria matamasha mbali mbali ya filamu yanayoandaliwa kama tamasha la kimataifa la filamu Zanzibar (ZIFF), European film Festival “EFF” lengo hasa likiwa ni kujifunza mbinu mbalimbali ambazo waongozaji wa ndani na wa nje ya nchi wanatumia kuongoza filamu.
2. Kuandika muswada wa filamu au kuigiza.
Kazi kubwa ya mwongozaji ni kuhakikisha anatengeneza filamu nzuri na yenye ubora wa kimataifa, akitumia vema vipaji vya waigizaji anaofanya nao kazi. Waongozaji wengi hasa wale wa Hollywood, bollywood walianza safari yao ya kuwa waongozaji kwa kuanza kuigiza, lengo lao likiwa ni kuijua vizuri tasnia ya uigizaji.
Ujuzi wa kuigiza unaweza kuwasaidia wale wote wanaopenda kuwa waongozaji wa filamu kujifunza mbinu na mitindo mbalimbali inayotumiwa na waongozaji mbali mbali kuongoza filamu, ni dhahiri kuwa kila mwongozaji wa filamu ana staili na mtindo wake wa kuongoza filamu.
Waongozaji wengi wazuri ni wale ambao historia yao pia ilianzia/ inaanzia kwenye uandishi wa muswada (script), mwandishi wa filamu ndie anayetengeneza taswira na mwongozo wa namna filamu itakavyokuwa, akipakingilia vizuri wahusika, maneno na matukio katika uandishi wake. tafiti zinaonyesha kwamba karibia waongozaji wote maarufu na bora wa filamu duniani ama kutoka Hollywood au Bollywood walishaandika/ wameandika miswada ya filamu mbalimbali kabla ya kuwa waongozaji, kwa mfano mwongozaji wa Hollywood Mery Gibson licha ya kuwa mwongozaji, ndiye aliiandika muswada wa filamu maarufu ya “Apocalypto” ya mwaka 2006.
3. Kupata taaluma ya filamu.
Taaluma si kitu ambacho watu wengi wanakitilia mkazo hapa kwetu Tanzania hasa kwenye tasnia ya filamu, ukweli utabakia kuwa kipaji pekee hakitoshi kumfanya mtu aweze kuwa mwongozaji bora, taaluma ni kitu cha msingi sana kukipata, waongozaji wote wa filamu duniani wamesomea taaluma ya uongozaji na ndio maana si ajabu kuona kila siku tunaona vitu tofauti na ubunifu wa hali ya juu katika filamu wanazoziongoza.
Waongozaji wengi hasa waliofanikiwa ni wale waliopata elimu ya stashahada au shahada kutoka katika vyuo , shule binafsi na vyuo vikuu zinatoa kozi za sanaa katika mambo ya utangazaji, redio, filamu na televisheni. Ingawa vyuo vingi tulivyonavyo vinatoa zaidi mafunzo ya nadharia katika tasnia ya sanaa, na vyuo vichache vinavyotoa mafunzo ya uongozaji wa filamu/sinema.
Wanafunzi katika kozi hizi wanajifunza namna ya kuwawasilisha ujumbe, upigazi wa picha, sauti, mwanga, uhariri,wanajifunza historia ya filamu na sinema, aina ya filamu kama zile zinazoelezea historia, za mapigano, mapenzi, za kisanyansi nk. Ni katika kozi hizi wanafunzi wanajadiliana uhalisia wa filamu na kuzichambua kwa kuangalia Fani na Maudhui..
4. kufanya kazi katika makampuni yanayotengeneza filamu.
Ujuzi ni kitu cha msingi sana katika kila kitu mtu anachofanya. Mtu anaweza kuwa mwongozaji bora wa filamu kwa kuangalia namna ambavyo utengenezaji wa filamu unavofanyika na nafasi hii mtu anaweza kuipaa kwa kufanya kazi na kampuni ambayo inajihusisha na utengenezaji wa filamu.ni hapo mtu anaweza kupata mafunzo ya nadharia na vitendo kwani atakuwa sehemu ambayo atajua namna ya kufanya kazi na wasanii na watu wengine wanaohusika katika utengenezaji wa filamu.
Ukweli ni kwamba hakuna njia hata moja kati ya hizo nne nilizoziainisha ambayo ni rahisi na nyepesi ya kumwezesha mtu kuwa mwongozaji bora filamu. Kama kweli umedhamiria na unataka kuwa mwongozaji fanya kazi ukijua hicho unachokifanya kinatoka moyoni na unamalengo nacho kwani safari ni ndefu, ngumu na yenye changamoto nyingi. Je uko tayari filamu yako kukataliwa na wachambuzi na wadau mbali mbali? Hapana, daima kuwa ni mtu mwenye mawazo na mtazamo chanya katika kila kitu unachojifunza na kuelekezwa. Njia bora na sahihi ya kuwa mwongozaji mzuri ni kuangalia filamu nyingi kadri uwezavyo na unapooana kitu kizuri chukua kalamu na karatasi kiandike, baadaye kitakusaidia.